Header Ads Widget

SOSOMA AELEZA CHANJO KWA WATOTO INAVYOWEZA KUWAEPUSHA NA MAGONJWA YA MLIPUKO, SHINYANGA YAVUKA LENGO

Mtoto akichomwa sindano ya chanjo. Picha na Mtandao

Na Damian Masyenene –Shinyanga 
MKOA wa Shinyanga umevuka lengo la utoaji chanjo kwa watoto chini ya mwaka mmoja baada ya kufanikiwa kuchanja watoto 78,247 sawa na asilimia 109 kufikia Septemba, mwaka huu kati ya walengwa 71,743 waliokusudiwa mwaka huu. 

Kwa mwaka jana (2019) mkoa huo ulifanikiwa kuchanja watoto 81,527 sawa na asilimia 115 kati ya walengwa 71,044 waliokusudiwa kuchanjwa. 

Hayo yalibainishwa jana Novemba 18, 2020 mjini Shinyanga na Mratibu wa Chanjo mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma katika mahojiano maalum na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake, ambapo alieleza kuwa mbali na chanjo hiyo ya watoto, pia wamekuwa wakitoa chanjo kwa akina mama wajawazito na chanjo ya HPV kwa ajili ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka 14. 

Ambapo, kwa takwimu za Septemba mwaka huu wametoa chanjo kwa asilimia 107 kwa dozi ya kwanza na asilimia 58 kwa dozi ya pili, huku changamoto zikielezwa kuwa mabinti wanashindwa kurudi kupata dozi ya pili kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kumaliza shule, kuhama ama kuolewa. 

Timoth Sosoma

Sosoma alisema kuwa kwa sasa nchini kupitia mpango wa taifa wa chanjo zinatolewa chanjo tisa ambazo zinakinga magonjwa 13, huku akieleza kuwepo kwa mwamko mkubwa wa jamii kupata chanjo hususan ya Penta, ambapo amesifu akinamama kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto na kwamba jamii inaendelea kuhamasishwa ili kuendelea kujitokeza zaidi. 

Akizungumzia umuhimu wa chanjo kwa watoto, Sosoma alieleza kuwa endapo jamii kubwa inakuwa haijapata chanjo, nafasi kubwa ya kupata magonjwa hasa ya mlipuko ni kubwa na usipopata chanjo unakaribisha magonjwa na ulemavu mfano kupooza, hivyo chanjo zimesaidia kupunguza magonjwa yakiwemo Ndui, Surua, Polio, Pepopunda, Kichocho na Kuhara. 

“Chanjo ni salama, jamii iaache kupuuza na kuzusha vitu vya hovyo kwa sababu hakuna kiongozi ama taifa ambalo litakubali kizazi chake kipewe kitu kibaya na kuangamizwa. Kwahiyo naomba wananchi wawapeleke watoto wapate chanjo kwa wakati. 

“Chanjo huongeza kingamwili, kukinga kuhara, kumfanya mtu kuwa na afya njema inayomkinga na magonjwa ya mlipuko, pia chanjo zimesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo kwa watoto na magonjwa ya mlipuko (magonjwa ya kuambukiza), hivyo ni jambo la msingi kama jamii itazingatia chanjo na kuzipata kwa usahihi,” alisema. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi wakati akifungua semina ya chanjo kwa wanahabari wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara iliyofanyika jijini Mwanza Septemba 4, 2020, baadhi ya magonjwa kama vile Polio, Surua na kuharisha yamekomeshwa kutokana na utoaji wa chanjo hizo, huku ugonjwa wa Polio ukiwa haupo nchini na Pepopunda kwa watoto wachanga mara ya mwisho uliripotiwa nchini mwaka 2012. 

“Watoto milioni 2 hadi 3 wameendelea kuokolewa kila mwaka kwa sababu ya utoaji chanjo salama na zilizothibitishwa, niwahakikishie kwamba chanjo zinazotolewa ni salama na zina manufaa kwa watoto wetu hali hii imesababisha vifo vya watoto kupungua, kwahiyo wazazi na walezi wawapatie watoto haki na wawapeleke katika vituo vya kutolea huduma wapate chanjo,” alibainisha. 

Naye Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Dafroza Lyimo akizungumza kwenye semina hiyo, alieleza kwamba chanjo inabaki kuwa njia rahisi na sahihi ya kumlinda mtoto na kuwa na familia yenye afya kwani baadhi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo husababisha ulemavu na vifo. 

“Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo yanasambaa kwa kasi kwenye jamii ambayo ina watu wengi ambao hawajapata chanjo, watu wasiopata chanjo wana nafasi kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya magonjwa kulinganisha na wale waliopata chanjo,” alisema. 

Wakizungumzia umuhimu wa chanjo, baadhi ya wananchi akiwemo Mariam John ambaye ni mzazi wa watoto watatu, alisema kuwa watoto wake wote walipata chanjo kwa usahihi na alikuwa akielimishwa umuhi mu wa chanjo, ambapo amewasihi wazazi kuzingatia maelekezo ya Serikali na kuacha kuzusha uvumi hasi juu ya chanjo zitolewazo kwa watoto. 

Naye Elisha Mussa akaiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao bado hawajafikiwa na elimu juu ya umuhimu wa chanjo ili kuondoa upotoshaji unaofanyika pale ambapo unafika wakati wa utoaji chanjo kwa watoto shuleni, kwani hali hiyo imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za serikali na kuwanyima fursa watoto hao kupata tiba. 

Post a Comment

0 Comments