Header Ads Widget

RC TELACK AKAGUA MADUKA, MAGHALA YA SARUJI, ATOA AGIZO KWA WAUZAJI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akikagua Saruji kwenye moja ya ghala mjini Shinyanga, jana.

Na Marco Maduhu, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, amebaini sababu za wafanyabiashara kupandisha bei ya Saruji mkoani humo, na kupiga marufuku kuuza bei ya juu.

Mfuko wa Saruji mkoani humo unaoanzia pointi 32 na 42, unauzwa kwa bei moja kuanzia Sh 20,000, 21,000 hadi 22,000, kwa wafanyabiashara wa maduka, lakini wenye maghala wanauza mfuko wa pointi 32 kwa Sh 17,500 na 42 kwa Sh 18,000.

Telack alibaini utofauti huo jana Novemba 18, 2020 alipofanya ziara ya kukagua bei ya Saruji kwenye maduka na maghala mbalimbali katika manispaa ya Shinyanga, kuwa Saruji ipo ya kutosha, isipokuwa kuna ujanja ambao unafanyika kwa wafanyabishara kutaka faida kubwa.

"Nimebaini kuna ujanja ambao unafanyika wa kuuza Saruji, wafanyabiashara wa kawaida wananunua Saruji kwa wenye maghara bei ya kawaida Sh 17,500 na 18,000, lakini wao wanapandishia wananchi na kuuza zaidi ya Sh 20,000," alisema Telack.

"Kuanzia sasa napiga marufuku kwa wafanyabiashara, hakuna kuuzia wananchi bei ya saruji kuanzia Sh 20,000 bali bei iwechini ,waache kutaka kupata faida kubwa na kuumiza wananchi," aliongeza.

Naye mmoja wa wafanyabiashara wa Saruji kwenye maduka mjini Shinyanga, John Ngalya, alikiri kupandisha bei ya saruji kwa madai ya kuuziwa bei ya juu kutoka kwa wanunuzi wakubwa wanaotoa Saruji moja kwa moja viwandani (mawakala).

Kwa upande wake wakala wa kusambaza Saruji kwa wafanyabiashara kutoka viwandani, Shufaa Mabula, alisema bei ya Saruji imepanda kutokana na uzalishaji kuwa mdogo tena wa oda na kusababisha kuingia gharama ya kusubiri mzigo.

Mmoja wa wananchi wa manispaa ya Shinyanga aliyezungumza na Shinyanga Press Club Blog juu ya kupanda kwa bei za saruji, Henry Michael, aliipongeza Serikali kwa kuingilia kati suala hilo ambalo limesababisha kupanda kwa gharama za ujenzi.
Mmoja wa mawakala wa kusambaza Saruji kutoka viwandani Shufaa Mabula (kushoto) akimuelezea mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack sababu za kupanda kwa bei ya Saruji.
Ukaguzi bei ya Saruji ukiendelea.


Post a Comment

0 Comments