Header Ads Widget

TUNZENI HAZINA YA WATOTO KUSTAWISHA TAIFA-DKT. JINGU

Katibu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu (kulia) akisalimiana na Mfadhili wa Kituo cha kulea watoto wadogo cha Neema Village cha Jijini Arusha Michael Fortson (kushoto) alipotembele kituoni hapo.

Na Mwandishi wetu, Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu ameitaka jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na kuwaandalia mazingira wezeshi ya kupata elimu.


Dkt. Jingu amesema hayo jijini Arusha alipotembelea vituo mbalimbali vya kulea watoto wadogo wanaokutwa katika mazingira magumu na hatarishi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vituo vya Neema Village, Amani na Makao ya Watoto ya St. Gabriel, Dkt. Jingu amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayotoa huduma ya kulea watoto wa aina hiyo, yanafanya kazi nzuri lakini yanawajibika kuzingatia kanuni, taratibu, sera na miongozo iliyopo ili kulinda maslahi ya taifa.

Amewataka watoa huduma kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza majukumu waliyokasimiwa ili huduma zao ziwe na tafsiri pana katika maendeleo ya nchi.

“Taarifa inaonesha kwamba mnafanya kazi nzuri, lakini kama wadau mnaoshughulika kukabiliana na ukatili, lazima mjue kuwa Ukatili ni jambo ambalo halikubaliki. Sheria zetu mbalimbali zinabainisha hususan dhidi ya watoto” alisema.

Amesema Serikali imeandaa mazingira mazuri ya kuwezesha utoaji wa huduma kwa Mashirika hayo kulingana na miongozo ambayo inalenga kulinda ustawi wa mtoto ambaye ni hazina kuliko hazina yoyote Duniani.

Amebainisha kuwa Arusha ni moja ya mikoa yenye tatizo kubwa la watoto wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi mitaani, hivyo ni wajibu wa Jamii kuhakikisha watoto wanaondolewa mitaani na kupelekwa shule.

Akizungumzia huduma zinazotolewa Neema Village, Mfadhili wa Kituo hicho Dorice Fortson amesema kituo kinajihusisha na huduma kwa walengwa ambao ni kuanzia watoto wanaokutwa kwenye mazingira magumu wakiwemo watoto waliofiwa na Wazazi, waliotelekezwa na wale wenye matunzo duni.

Dorice ameongeza kuwa Kituo hicho pia kinatoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wanaoishi katika mazingira magumu na kuwafundisha mbinu za kujitegemea kupitia miradi mbalimbali baada ya kupata mafunzo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Amani Irene Wampembe amesema pamoja na changamoto kadhaa zilizopo kituo kimeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa watoto wapatao 55 tangu kuanzishwa kwake ambapo kati yao watoto 33 wameunganishwa na familia zao.

Aidha, Irene ameshukuru kwa huduma zinazoendelea kutolewa na maafisa Ustawi wa Jiji la Arusha, Halmashauri na Mkoa na Serikali kwa ujumla kwa kuanzisha mpango wa nyumba salama kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika vitendo vya ukatili.

Awali akitoa taarifa kuhusu hali ya watoto na Ustawi wao, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Wedsm Sichwalwe amesema tatizo la vitendo vya ukatili kwa watoto sio la kufumbia macho na linaweza kuwa mzigo mkubwa hapo baadaye.

Aidha, Dkt, Sichwalwe amesema hivi sasa kuna mahitaji makubwa ya huduma za ustawi nchini sambamba na kuendelea kuboresha miundombinu ya Sekta ya afya ili kuendana na mabadiliko na mahitaji ya huduma katika sekta hiyo.

 Katibu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akisalimiana na Mtoto Maria katika Kituo cha kulea watoto cha Neema Village Jijini Arusha alipotembele kituoni hapo.
Katibu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akiangalia picha mbalimbali za watoto walionufaika na huduma ya malezi katika kituo cha kulea watoto cha Neema Village Jijini Arusha, alipotembelea kituoni hapo.
Katibu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu (kulia) akisalimiana na Sister Flora Ndwatwa, Meneja wa Kituo cha malezi ya Watoto ambao wazazi wao ni wafungwa au Mahabusu kilichoko Jijini Arusha.