Header Ads Widget

TCRA, COSOTA ZAENDESHA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KANDA YA ZIWA JUU YA HAKIMILIKI, MAUDHUI YA KIMTANDAO NA UTANGAZAJI


Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Fransic Mihayo (kulia) akiwasilisha mada mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya utangazaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo Agosti 10, 2020.


Na Damian Masyenene- Shinyanga Press Club Blog, Mwanza 
KATIKA kuongeza ufahamu juu ya maboresho ya sheria mpya za utangazaji, uchapishaji maudhui mtandaoni na kanuni mpya za hakimiliki, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Miliki nchini (COSOTA) zimeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya utangazaji kutoka mikoa mbalimbali ya kanda hiyo. 

Mafunzo hayo yamefanyika leo Agosti 10, 2020 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza yakiwahusisha wawakilishi zaidi ya 100 kutoka vyombo mbalimbali vya habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa. 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo, amesema elimu hiyo ni kuwasaidia watoa mahudhui nchini kuyafahamu mabadiliko ya sheria za utangazaji, sheria ya utoaji wa huduma mtandaoni, kanuni mpya za uchaguzi za mwaka 2020 na maboresho ya kanuni za haki miliki 

Mhandisi Mihayo amesema mabadiliko kwenye kanuni za maudhui ya kimtandao za mwaka 2020 zilizoanza kutumika Julai Mosi, mwaka huu zimelenga kuboresha huduma za maudhui mtandaoni na usimamizi wake, ambapo ameyataja baadhi ya maudhui yaliyozuiliwa kuingia mtandaoni kuwa ni ya ngono, maisha binafsi ya mtu na kuheshimu utu wa mtu, usalama wa taifa na ukiukwaji wa sheria, biashara haramu, afya na usalama wa raia, haki miliki, dini na taarifa za uchochezi zinazoweza kuvuruga amani. 

“Sheria imeshaanza kutumika tangu Julai mosi, mwaka huu, kwahiyo sitegemei muendelee kukiuka kanuni hizi, yale maudhui yanayorushwa wewe ndiyo kiranja, tujikite kufuata utaratibu uliowekwa. 

“Tunajua kabisa kuna vyomb o vitaanza saa 5, kwahiyo tutii sheria, naomba tukaangalie vizuri kwenye mambo ambayo yameainishwa ambayo hayatakiwi kuchapishwa, ili tusijiweke matatizoni,” amesisitiza. 

Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano wa TCRA Makao Makuu, Herieth Shija, akiwasilisha mada juu ya maboresho ya kanuni mpya za matangazo ya Redio na Television ya mwaka 2020, amesema miongoni mwa maboresho ni vipindi vya watu wazima visivyopaswa kusikilizwa na watoto vianze kuruka kuanzia saa 6 usiku hadi 11 alfajiri tofauti na hapo awali vilipokuwa vinaruka kuanzia saa 4 usiku. 

Vile vile, Hellen amesema chombo cha habari cha ndani ya nchi hakipaswi kujiunga na chombo kingine cha nje na kurusha matangazo bila kupata kibali kutoka TCRA, ambapo mwenye leseni ya kurusha maudhui hapaswi kufanya biashara ya matangazo/biashara ya maudhui na mtu kutoka nje bila kuambatana na afisa wa serikali ama mtumishi wa TCRA. 

Naye Mhandisi Mwandamizi TCRA Kanda ya Ziwa, William Mnyipembe akizungumzia kuhusu namna vyombo vya habari vinavyopaswa kuendesha shughuli zake wakati wa uchaguzi, mbali na mambo mengi yanayopaswa kuzingatiwa, mwajiriwa yeyote wa kituo (mtangazaji) anayetaka kujihusisha na siasa, ni lazima aende likizo, aache kazi ama apumzike wakati wa mchakato wa uchaguzi. 

“Utoaji taarifa siku ya uchaguzi ni lazima vituo vya habari vihabarishe kile walichokiona, wasitegemee taarifa za kuambiwa ama maoni yao bali kile walichokiona eneo ambalo kura zinapigwa, pia waepuke kutoa mambo ambayo ni ya kufikirika na taarifa zenye kusudi la kuchafua mtu. 

“Wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi, tuhakikishe matokeo unayoyatangaza ni sahihi na hakika kutoka mamlaka zilizokasimiwa kutoa matokeo, tusitegemee kusema kwamba tunakusanya taarifa kutoka kwenye vituo alafu tunajumlisha sisi wenyewe kwa weledi wetu, hivyo Sisi tusiwe watoaji wa matokeo,” amesema. 


Mwanasheria kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Lupakisyo Mwambinga ameeleza juu ya marekebisho ya kanuni za utangazaji, maonesho na maudhui kwa umma yaliyofanyika yanayoeleza namna vyombo vya habari vitakavyolipa mirabaha kwa kazi za wasanii zinazochezwa, ambapo watoa huduma za habari hasa redio na televisheni wametakiwa kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha kanuni hizo na kuleta faida kwa pande zote mbili.
 Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Fransic Mihayo


 Afisa Mawasiliano TCRA, Harieth Shija akiwasilisha mada katika mafunzo hayo
 
Mhandisi Mwandamizi kutoka TCRA Kanda ya Ziwa, William Mnyipembe akiwasilisha mada mbalimbali za maboresho ya kanuni na sheria za uchapishaji maudhui mitandaoni na vituo vya utangazaji

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru (kulia) na wawakilishi kutoka Shinyanga Press Club Blog, Damian Masyenene na Josephine Charles wakifuatilia mafunzo hayo
 
Wawakilishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari mikoa ya Kanda ya Ziwa wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa
 
Wanahabari na viongozi wa vituo vya utangazaji kutoka Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo
 
Mafunzo yakiendelea
 
Mafunzo yakiendelea katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza 
 
Washiriki wakifuatilia mafunzo
 
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wilayani Kahama nao walikuwa sehemu ya mafunzo hayo

Wawakilishi kutoka Shinyanga Press Club Blog wakifuatilia mafunzo hayo

PICHA ZOTE NA KADAMA MALUNDE