TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp +255 789 632 732, +255 756 546 015 au +255 686 057 440

MENEJA WA TARURA SHINYANGA ASIMAMISHWA KAZI KWA UTENDAJI DHAIFU, DC MBONEKO APONGEZA


Daraja la kuunganisha shule ya msingi Bugweto likiwa katika hali isiyo ridhisha.

Na Shinyanga Press Club Blog

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa  Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, amemsimamisha kazi Meneja wa Tarura Manispaa ya Shinyanga, Jolister Mtelani, kwa kushindwa kusimamia vizuri matengenezo ya madaraja, pamoja na kuwabana wakandarasi kumaliza kazi zao kwa wakati, huku wakijenga madaraja chini ya kiwango.

Mtelani amesimamishwa kazi leo wakati Mtendaji huyo Mkuu wa Tarura alipofanya ziara ya kukagua matengenezo ya madaraja kwenye baadhi ya maeneo katika Manispaa ya Shinyanga ikiwemo miundombinu ambayo iliharibiwa na msimu wa mvua uliopita.

Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff amesema hajafurahishwa na utendaji kazi wa Meneja wa Tarura Manispaa ya Shinyanga, Jolister Mtelani hivyo kuamua kumsimamisha kazi, huku kiti chake akikaimishwa Meneja Tarura wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambaye atasimamia matengezo ya barabara na madaraja manispaa hiyo hadi pale atakapoletwa meneja mwingine.

"Nimemsimaisha kazi meneja wa Tarura manispaa ya Shinyanga, baada ya kuona utendaji wake kazi siyo mzuri, ambapo ameshindwa kabisa kusimamia matengenezo barabara na madaraja, pamoja na kuwabana wakandarasi kumaliza kazi kwa wakati huku wakiyajenga chini ya kiwango," amesema Seff.

"Pia mkandarasi ambaye anatekeleza miradi hii ya ujenzi wa madaraja, asipewe kazi tena zijazo, na taarifa zake nipewe ili nizi ripoti kwenye bodi ya wakandarasi," ameongeza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amepongeza hatua iliyochukuliwa ya kusimamishwa kazi Meneja wa Tarura, na kubainisha kuwa alishawaonya kufanya kazi kwa uzembe kwa kutekeleza miradi chini ya kiwango na kuwabeba wakandarasi ambao hawana sifa.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miundombinu mbalimbali kwa wananchi zikiwamo barabara na madaraja, lakini kuna baadhi ya watumishi bado wanafanya uzembe kuisimamia miradi hiyo.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Mtendaji Mkuu wa Tarura nchini, Victor Seff, akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua ujenzi wa matengenezo wa madaraja katika manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akizungumza mara baada kumaliza ziara ya kukagua ujenzi na matengenezo ya barabara katika wilaya hiyo wakati wa ziara ya Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff.

Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff, akikagua nguzo ya daraja lilopo Bugweto manispaa ya Shinyanga kwenda Itilima wilayani Kishapu, ambapo ujenzi wake ni wa kusuasua ukidaiwa pia kujengwa chini ya kiwango.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akikagua nguzo ya daraja lilopo Bugweto manispaa ya Shinyanga kwenda Itilima wilayani Kishapu.

Ukaguzi wa nguzo ya daraja ukiendelea

Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff (alisimama mbele) pamoja na watendaji wengine wa serikali wakilitazama daraja likiwa limezibwa na kichuguu na kushindwa kupitisha maji.


ukaguzi wa madaraja ukiendelea

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akimuonyesha Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff (wa kwanza kushoto) daraja lililopo katika kijiji cha Lyandu Kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga ambalo halifanyi kazi tena.

Ukaguzi wa madaraja ukiendelea.

Ukaguzi wa madaraja ukiendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akiangalia mchanga ambao ambao hauna kiwango unaotumika kwenye matengenezo ya madaraja wilayani humo

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akitazama kokoto ambazo zinatumika kwenye matengenezo ya madaraja wilayani humo.

Meneja wa Tarura Manispaa ya Shinyanga, Jolister Mtelani (kushoto) akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko wakati wa ziara ya Mtendaji Mkuu wa Tarura, Mhandisi Victor Seff kukagua miradi mbalimbali ya barabara na madaraja wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akisaidiana na wananchi kukata Matobolwa, (viazi vilivyopikwa) na kuwapongeza wanawake kwa kujituma kufanya kazi.

Muonekano wa viazi vilivyopikwa ambavyo vinatengenezwa matobolwa.
Picha na Marco Maduhu