Header Ads Widget

WAZIRI LUKUVI NAE ACHUKUA FOMU ISIMANI, MPINA AELEZA SABABU ZA KUITAKA TENA KISESA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amefika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Ismani mkoani Iringa.
Lukuvi amewasili ofisi za chama hicho akiwa ameambatana na mkewe.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametaja sababu zilizomsukuma kuwania tena ubunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa Simiyu baada ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15 kwa mafanikio makubwa huku akibainisha kuwa kazi ya kusaka maendeleo katika jimbo hilo bado haijakamilika.

Akizungumza nje ya Ofisi Kuu ya CCM Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kuteuliwa kugombea Jimbo la Kisesa, Waziri Mpina amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumruhusu kuchukua fomu hiyo na kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kuendelea kumuunga mkono katika safari hiyo.

“Naamua kuchukua fomu ya kugombea Jimbo la Kisesa kwa sababu kazi ya kusaka maendeleo ya jimbo bado haijakamilika,”amesema Waziri Mpina.


 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi na Uvuvi, Luhaga Mpina (kushoto) akipokea fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea Ubunge Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu. kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Charles Dotto Mazuri. Amechukua fomu leo, Julai 15, 2020


Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Charles Mazuri hadi kufikia Julai 15 saa saba mchana jumla wa watia nia nafasi ya ubunge kwa Jimbo la Kisesa walikuwa wamefikia tisa, akiwemo Waziri Mpina na Mbunge anayemaliza muda wake.

Mazuri amesema kwa upande wa jimbo la Meatu jumla ya wagombea 11 wamejitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho na kufanya idadi ya wagombea 20 wanaowania nafasi hiyo kwa majimbo yote mawili.