Header Ads Widget

HALMASHAURI ZA KAHAMA MJI NA MSALALA ZAKABIDHIWA SH BIL. 1.5 KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (wa pili kutoka kulia) akipokea hundi ya Sh Bilioni 1.5 kutoka Twiga Minerals Corporation Ltd zilizokabidhiwa na Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto). katikati ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba na kulia ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila.

Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
Halmashauri za Mji wa Kahama na Msalala zimekabidhiwa hundi zenye thamani ya Sh Bilioni 1,535,821,894.85 kama malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia Januari hadi Juni, 2020 kutoka Kampuni ya Uchimbaji madini ya Twiga Minerals kupitia migodi yake ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu.

Ambapo Mgodi wa Buzwagi umelipa Sh Bilioni 1,159,817,107.83 kwa halmashauri ya Mji wa Kahama, huku mgodi wa Bulyanhulu ukilipa Sh Milioni 376,004,787.02 kwa halmashauri ya Msalala.

Malipo hayo yanafanyika ili kutekeleza hitaji la kisheria lakini pia ikiwa ni sehemu ya mikataba ya makubaliano kati ya migodi hiyo miwili na halmashauri husika ambayo inalenga kuboresha utoaji wa huduma katika jamii zinazozunguka migodi hiyo katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya na upatikanaji wa maji safi na salama.

Zoezi la kukabidhi hundi hizo limefanyika leo Julai 15, 2020 mjini Kahama katika ofisi za Halmashauri ya Mji wa Kahama likihudhuriwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Annamringi Macha, Mkurugenzi wa Mji wa Kahama, Anderson Msumba pamoja na Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo, Joachim Simbila.
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha

Akipokea hundi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha amesema malipo hayo ya ushuru ni zao la kwanza la ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick, ambapo kutokana na makubaliano hayo wilaya hiyo imeanza kupokea ushuru huo na fedha za kurudisha kwa jamii (CSR) kwa kiwango kikubwa kuliko awali, huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika utaratibu ulio bora.

“Kupitia fedha hizi tayari miradi mbalimbali imeanza kuibuliwa ikiwemo ujenzi wa jingo la wagonjwa wan je (OPD) na kliniki zitakazogharimu Sh Bilioni 3.2 na miradi mingine ya maji, pia halmashauri ya Kahama imeendelea kubuni miradi mbalimbali yenye tija kwa maendeleo ya vijana, wenye ulemavu na wanawake.

“Kwa upande wa halmashauri ya Msalala tumekaa na vikundi mbalimbali katika kata zinazozunguka migodi hii ambapo Sh Milioni 900 zimetengwa kusaidia maendeleo ikiwemo ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike,  kuimarisha kituo cha afya Bugarama, huduma za maji na miradi mingine ya maendeleo itakayowagusa moja kwa moja wananchi,” amesema Macha.

Akifafanua kuhusu malipo hayo, Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, Benedict Busunzu amesema migodi ya Twiga Minerals chini ya Kampuni ya Barrick Tanzania hulipa ushuru wa huduma kila baada ya miezi sita kwa halmashauri ambazo migodi yao inaendesha shughuli zake kulingana na mapato yao ya kila mwaka.

“Licha ya kulipa kodi stahiki bado tumekuwa tukijishughulisha kuhakikisha migodi yetu inakuwa mdau muhimu wa maendeleo kupitia sera yake ya maendeleo kwa jamii ili kuunda fursa endelevu za kiuchumi na maendeleo kwa ujumla kwa jamii zinazozunguka migodi ya Barrick na kuinua uchumi wa wilaya pamoja na kuboresha ustawi wa maisha ya wenyeji, lengo ni kuona mamlaka husika zinaelekeza fedha hizi katika miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yanayotuzunguka,” alisema.

Katika hatua nyingine, Busunzu ameeleza kuwa wameendelea kutekeleza sera ya maendeleo kwa jamii, ambapo kwa mwaka jana mgodi wa Buzwagi ulitenga Sh Bilioni 2.3 kwa kuwekeza katika jamii kuboresha huduma mbalimbali, huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono na kwamba kupitia uwepo wao wananchi wataendelea kunufaika zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila amewahimiza viongozi wa halmashauri husika zilizopokea fedha hizo kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa wananchi wa maeneo lengwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akizungumza baada ya kupokea hundi hizo.

 Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu akizungumza baada ya kuzikabidhi halmashauri za Mji wa Kahama na Msalala hundi ya Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika jamii inayoizunguka migodi hiyo.
 Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila
 Viongozi wa Halmashauri ya Msalala wakifurahia baada ya kupokea hundi ya Sh Milioni 376, 004,787 kutoka  mgodi wa Bulyanhulu
 Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba (katikati) wakipokea hundi ya Sh Bilioni 1,159,817,107 kutoka mgodi wa Buzwagi iliyokabadhiwa na Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege (katikati) akipokea hundi ya Sh mMilioni 376,004,787 kutoka kwa Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto) na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha