Header Ads Widget

BILIONEA LAIZER AWATAKA WATANZANIA WENGI KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA MADINI

Bilionea wa Tanzanite, Laizer Saniniu amewataka watanzania kujitokeza kwenye uchimbaji wa madini ya Tanzanite kwa kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira mazuri  ya uwekezaji kwenye Sekta ya Madini.

Bilionea Saniniu ameyasema hayo leo tarehe 12 Julai, 2020 mara baada ya kufanya ziara kwenye Banda la Tume ya Madini na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akielezea siri ya mafanikio kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya Tanzanite katika eneo la Mirerani lililopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara Bilionea Saniniu alisema kuwa ni kutokana na usimamizi mzuri wa Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwenye usimamizi wa  shughuli za uchimbaji na uuzaji wa madini ya Tanzanite katika eneo hilo.

“Mara baada ya Serikali kuweka ukuta wa Mirerani, kumekuwepo na usalama wa kutosha huku wachimbaji wadogo wa madini wakiuza madini yao kwa bei inayoendana na Soko la Dunia na ya uhakika huku ikiimarisha ulinzi katika eneo la Mirerani,” alisema Saniniu.

Saniniu aliendelea kusema kuwa, amejipanga kuendeleza biashara ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite kwa kununua vifaa vya kisasa na kutoa ajira zaidi kwa wananchi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Saniniu alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwenye usimamizi wa shughuli za uchimbaji wa madini ya Tanzanite huku kodi mbalimbali zikilipwa Serikalini.

“ Serikali imekuwa na msaada mkubwa kwetu, pasipo ukuta wa Mirerani ningeweza kuibiwa mawe ya Tanzanite yaliyopatikana, lakini nashukuru  mara baada ya wataalam kutoka Tume ya Madini kuyathaminisha, nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufaya biashara na Serikali,” alisema Saniniu.

Wakati huohuo akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya mbali na kumpongeza Bilionea Saniniu alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wanakuwa mabilionea kwa kuwapa mbinu za kisasa za uchimbaji wa madini.

“Nitoe wito kwa wachimbaji wa madini wasio rasmi kuomba leseni za madini na kuanza kuchimba madini, na sisi kama Tume ya Madini kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, tupo tayari kuwasaidia ili waweze kunufaika,” alisema Profesa Manya.

Akielezea mikakati ya Serikali kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini nje ya nchi, Profesa Manya alieleza kuwa mbali na uanzishwaji wa masoko ya madini 28 pamoja na vituo vya ununuzi wa madini 28 nchini na ujenzi wa ukuta wa Mirerani, Serikali imeweka maafisa kwenye mipaka ya nchi pamoja na viwanja vya ndege.

Aidha, Profesa Manya aliwataka wachimbaji wa madini nchini kufuata sheria ya madini pamoja na kanuni zake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.