Header Ads Widget

SIMBA YAICHAPA YANGA 4-1, SASA KUCHEZA NA NAMUNGO FAINALI SUMBAWANGA


Kiungo wa timu ya Simba, Gerson Fraga akishangilia kwa kunyoosha mikono juu baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza.
Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
TIMU ya Simba SC leo imefanikiwa kusonga mbele na kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu kama Kombe la FA, baada ya kuwachapa watani wao wa jadi, Yanga SC kwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa leo saa 11 jioni katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba wameingia kwa nguvu kubwa katika mchezo huo wakihitaji kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu Machi, mwaka huu, ambapo wameutawala mchezo huo wakitandika kandanda safi na kupoteza matumaini ya wapinzani wao kupata ushindi.

Mabao ya Simba yamefungwa na Gerson Fraga mnamo dakika ya 20, Cloutous Chama (50), Louis Miquissone (52) na Mzamiru Yassin (88), huku bao la kufutia machozi la Yanga likipachikwa nyavuni na Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika dakika ya 71.
Mchezaji wa Simba, Mzamiru Yassin akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la nne.

Kufuatia ushindi huo, Wekundu wa Msimbazi Simba watakutana na Namungo FC ya Lindi katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2020 katika uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Namungo FC ambao ni msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu, walitinga hatua ya fainali jana Julai 11, 2020 baada ya kuwanyuka Sahare All Stars kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.