Header Ads Widget

SHIRIKA LA MAPERECE LAWAFUNDA MABALOZI 37 WA FISTULA UKEREWE KUIBUA NA KUSAIDIA WAHANGA



Mabalozi wa Fistula wakifuatilia kwa umakini mafunzo 

Na Mwandishi Wetu – Shinyanga Press Club Blog 
KATIKA kuhakikisha wahanga wa ugonjwa wa Fistula wanaibuliwa, kuelekezwa kwenye matibabu na kupatiwa msaada wa kisaikolojia, wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo mabalozi 37 wa tatizo hilo wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza. 

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Shirika la MAPERECE la wilayani Magu mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na AMREF na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando mahususi kwa mabalozi hao 37 ambao ni watoa elimu ngazi ya jamii na watoa tiba za asili lengo likiwa ni kuwawezesha kutimiza majukumu yao katika kuibua wahanga wa Fistula, kuwaelekeza kwenye matibabu na kuwapatia msaada wa kisaikolojia. 

Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ukerewe, Cecilia Oswago amewataka mabalozi hao kutumia mafunzo hayo kuhakikisha lengo la kutoa elimu na kupunguza madhara ya ugonjwa wa fistula ya uzazi kwa wanawake na kuwaibua waathirika wote na kuwafikisha kwenye matibabu. 

Mratibu wa Mradi wa mafunzo hayo kutoka Shirika la Maperece, Revitus John ameeleza kuwa ugonjwa wa fistula ya uzazi unaathari nyingi kwa wanawake ikiwemowa kushuka moyo, kunyanyapaliwa, kutengwa, kukatalia na kujiua, hivyo akawataka mabalozi hao kuwafikia wanawake hao na kuwabaini na kuwapa elimu na msaada kisaikolojia itakayowasaidia na kujua kuwa ugonjwa huo unatibika. 

Pia amebainisha kuwa kwa kushirikiana na shirika la AMREF na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, wagonjwa wa Fistula wote wataweza kupata matibabu bila gharama yoyote kwani wafadhili kwa kushirikiana na serikali wamejitoa kuhakikisha ugonjwa unakoma. 

Kwa upande wake Mtaalamu wa magonjwa ya Fistula kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk. Reolvin Elishaphat ameeleza kuwa Fistula ya Uzazi (Obstetric fistula) ni tundu lisilo la Kawaida ambalo halikutakiwa kuwapo kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke (Vesico-Viginal Fistula-VVF) ambapo wanawake wengi hupata VVF, wachache hupata RVF na wachache zaidi hupata zote kwa pamoja. 

“Ugonjwa wa Fistula ya Uzazi ni tatizo la nchi zinazoendelea na halipo tena katika nchi zilizoendelea ambapo takribani akina mama Milioni mbili wanaishi na fistula duniani, akina mama 50,000 hadi 100,000 wanapata fistula kila mwaka. Inakadiriwa kila mwaka kuna wagonjwa 3,000 wapya wa fistula Tanzania wanatibiwa kwa mwaka ambapo wagonjwa 1,600 wanabaki bila matibabu,” alisema Elishaphat. 

Alivitaja baadhi ya visababishi vya Fistula ya Uzazi kuwa ni uchungu pingamizi kwa muda mrefu kabla ya kupata msaada wa kitaalamu unaoleta makazo na kuzuia damu kupita na kasha kusababisha tundu, upasuaji wakati wa uzazi, matibabu kupitia mionzi hasa kwenye matibabu ya magonjwa kama ya Saratani kwenye sehemu ya nyonga na shingo ya kizazi, miundombinu mibovu kupelekea kuchelewa kufika katika vituo vya afya, ucheleweshaji ngazi ya familia na vituo vya afya pamoja na majeraha na magonjwa ya kifua kikuu na kibofu cha mkojo. 

Mwakilishi kutoka shirika la AMREF, Dk. Magdalena Dhalla ameelezea baadhi ya dalili za mgonjwa mwenye Fistula kuwa ni kutokwa na haja ndogo au kubwa usiku na mchana bila kujitambua, vidonda sehemu ya siri, harufu mbaya ya mkojo au kinyeesi na kuchechemea kwa sababu ya kuumiza mguu kutokana na uchungu pingamizi. 

“Madhara mengine yanayoambatana na ugonjwa wa Fistula ya uzazi ni kupoteza uwezo wa kuzaa tena, kukosekana kwa kushiriki tendo la ndoa, kuporomoka kiuchumi, Hivyo ni vema wagonjwa wakafika hospitali kwa matibabu na ugonjwa huu unatibiwa bure ikiwa ni pamoja na operesheni katika hospitali ya rufaa Bugando au CCBRT,” alisema Dk. Dhalla. 
Mwakilishi kutoka shirika la AMREF, Dk. Magdalena Dhalla akitoa elimu kwa washiriki 

Mmoja wa wahanga wa ugonjwa wa Fistula kutoka wilayani Ukerewe, Vaileth Deus ameeleza kuwa baada ya kujifungua mtoto wake wa Saba alipatwa na ugonjwa huo ambapo alianza kutokwa na haja bila kujua. 

“Nilichelewa sana kufika hospitali kupata huduma ya kujifungua baada ya kuanza kupata uchungu lakini baada ya matibabu hospitali ya wilaya Nansio nilipewa rufaa na nikapelekwa Bugando ambapo nilifanyiwa upasuaji na nilikaa huko takribani miezi 8 na niligharamiwa matibabu bure na nauli ya usafiri kurudi nyumbani,” alisema Vaileth. 

Mratibu wa ugonjwa wa Fistula wilaya ya Ukerewe, Crispine Theobald amelishukuru shirika la MAPERECE kwa jitihada hizo kwani wanawake wengi ambao walipoteza matumaini juu ya kutibiwa na kupona ugonjwa wa Fistula kwa sasa wanapokelewa hospitali ya wilaya na kupewa rufaa kwenda Bugando ambapo gharama zote za matibabu ni bure, huku akiwataka wananchi kuondokana na mila potofu juu ya ugonjwa huo kwamba unasababisha na kurogwa. 
Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo akitoa elimu kwa mabalozi wa fistula wilayani Ukerewe 
Baadhi ya mabalozi wa ugonjwa wa Fistula ya uzazi kwa wanawake wilayani Ukerewe wakifuatilia mafunzo 
Mafunzo yakiendelea