Header Ads Widget

WADAU WAZIDI KULIA NA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971 VITA DHIDI YA NDOA ZA UTOTONI



Mkurugenzi wa Shirika la Agape ambalo linatetea haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga , John Myola akielezea namna Sheria ya ndoa ilivyo kikwazo kutomeza mimba ndoa za utotoni.

Na Marco Maduhu, Shinyanga 
SHERIA ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi, na 15 Mahakama, imetajwa kuwa tatizo kukomesha mimba na ndoa za utotoni. 

Mkurugenzi wa Shirika la Agape linalotetea haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, John Myola alibainisha hayo jana kwenye ziara ya machampion wa kupambana na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, walipotembelea watoto ambao ni wahanga wa matukio hayo katika Shirika la Agape, ziara iliyoandaliwa na Shirika la Msichana Intiative.

Amesema moja ya changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo katika mapambano ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga, ni Sheria hiyo ya ndoa ya mwaka 1971, ambayo imekuwa ikisababisha wahusika kutofungwa jela na kuwa fundisho kwa wengine sababu ya kuruhusu mtoto chini ya miaka 18 kuolewa.

"Mfano kuna kesi moja ambayo tulitibua ndoa ya mwanafunzi, lakini ilipofika Mahakamani Hakimu akasema hapo hakuna kesi, sababu ndoa hiyo imeridhiwa na wazazi wake, na wamesha chukua mahari na wameshiriki kwenye harusi, kesi ndio ikaishia hapo na mwanafunzi akazima ndoto zake," amesema Myola.

Naye mmoja wa machampion, Aida Kenani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini , amesema kuna haja kubwa ya Sheria hiyo ya ndoa kufanyiwa marekebisho ya haraka ili kumlinda mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.

Aidha akizungumza na watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni wanaolelewa na Shirika la Agape, amewataka wasikate tamaa, bali wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao ambazo zilizotaka kuzimwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeka Gyumi, ambao wanatetea haki za watoto, amesema wamefanya ziara hiyo na machampion ili kujifunza, kubadilisha uzoefu na kuchukua changamoto, ambazo ni tatizo kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, ili ziendelee kutafutiwa ufumbuzi.

Pia amewataja machampion wengine wa kupambana kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ambao aliaambatana nao, kuwa ni Mbunge mwakilishi wa vijana taifa kutoka mkoani Mwanza, Ng'wasi Kamani na aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2005 Nancy Sumari pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu Tanzania, Shamimu Khan.


Afisa Miradi kutoka Shirika la Agape, Peter Amani akizungumza kwenye kikao hicho cha Machampioni na watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.

Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Kenani, akielezea namna alivyoguswa na mikasa ambayo walifanyiwa watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni, wanaolelewa na Shrika la Agape.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Waislam Tanzania, Shamimu Khan, akiwasihi watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni wanaolelewa na Shirika la Agape kuwa wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Intiative, Rebeka Gyumi, akielezea lengo la ziara yao na Machapioni Mkoani Shinyanga pamoja na kutembelea watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu Tanzania, Shamimu Khani (kushoto), Aliyekuwa Miss Tanzania Mwaka 2005, Nancy Sumari (katikati) na kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Intiative, Rebeka Gyumi wakiwa kwenye Shirika la Agape ambalo linalea watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.

Machampioni wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, ambao ni wabunge wakiwa kwenye shirika la Agape linalolea watoto ambao ni wahanga wa matukio hayo, kulia ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kasikazini Aida Kenani, akiwa na Mbunge Mwakilishi wa Vijana Taifa kutoka mkoani Mwanza Ng'wasi Kamani.


Post a Comment

0 Comments