Header Ads Widget

RAIS ATAKA KUREJESHWA IMANI YA WAWEKEZAJI TANZANIA, AONYA URASIMU NA MABAVU....AGUSA UTOROSHAJI TANZANITE

Rais Samia Suluhu Hassan

Na Damian Masyenene
RAIS Samia Suluhu Hassan amewaagiza Waziri wa Uwekezaji, Geofrey Mwambe na wa Biashara na Viwanda, Prof. Kitila Mkumbo, kuondoa vikwazo, urasimu, na mabavu katika kushughulikia uwkezaji nchini ili kuhakikisha nchi inarejesha imani kwa wawekezaji.

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, ambapo amesisitiza kuwa kutokana na urasimu katika utoaji vibali vya kazi na matumizi ya nguvu katika kudai kodi na kutoa leseni za uwekezaji, kumewafanya wawekezaji wengi kufunga biashara na kukimbia.

"Wanaosimamia vibali vya kazi wamegeuka waungu watu na imekuwa fursa yao kuchuma….kwanini muwalazimishe wawekezaji waweke watu ambao hawawataki na hawana uwezo, mnaosimamia sekta hiyo mkaweke mazingira mazuri, tunataka wawekezaji wafurahie mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania.

"Makampuni yanafungwa ndugu zangu siyo uongo, ajira nyingi zinapotea na mzunguko wa fedha unapotea," amesema.

"Wawekezaji wanalaumu sana Urasimu wa Serikali ya Tanzania, naomba sana mnaosimamia uwekezaji (Mkumbo na Mwambe mkalifanyie kazi, Mwambe wewe ni mmoja wa waliotengeneza huo urasimu sasa mwende mkarekebishe,"
ameeleza.

Rais Samia ameeleza kuwa mfumo wa utozaji kodi nchini dhidi ya wawekezaji umekuwa hautabiliki na hakuna mfumo unaoeleweka wa kodi kwa wawekezaji, hali ambayo imekuwa ikiwawia vigumu wawekezaji kuendelea na shughuli zao.

"Hatutabiriki na kodi zetu kwa wawekezaji. Nawataka mkarekebishe hayo, Watu wanataka kuwekeza Tanzania lakini kwa mambo yetu watu wanakimbia Tanzania, tunataka watu warudi wawekeze Tanzania. Naomba sana tukapunguze misuli kwenye masuala haya ya uwekezaji, tukarudishe imani ya wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania," amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amegusia sekta ya madini na kutaka kasoro na mapungufu yaliyopo yarekebishwe, ambapo amebainisha kuwa bado kuna utoroshaji wa madini ya Tanzanite eneo la Mererani, licha ya Serikali kujenga ukuta mkubwa na kuimarisha ulinzi.

"Licha ya ukuta na ulinzi bado madini yanatoroshwa kama mwanzo, jeshi linalinda juu watu wanatorosha chini kwa chini. Kitalu C kimetengwa kama akiba lakini kimeanza kuguswa, naomba kiacheni kina matumizi yake," ameagiza.

"Nyinyi ndiyo injini, tunawategemea kufikisha gurudumu letu. Kwenda kwetu kwa kasi ama kuzorota kutawategemea nyinyi, mkafanye kazi na kuwatumikia watanzania bila bugudha, mkawe neema na siyo kero na nuksi, mkasimamie haki na siyo dhuluma," amesema. 

Awali Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amewaasa makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi wapya walioapishwa kuhakikisha wanasimamia uhamisho wa fedha ambao hauna sababu, udanganyifu miradi ya maendeleo, matumizi ya fedha ambayo siyo mazuri, huku akiwaagiza kuangalia matumizi ya magari, Mafuta na matengenezo kwani huko kuna tatizo kubwa.

Naye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wateule hao wapya kusoma majukumu na kazi za nafasi zao, waelewe miradi inayotekelezwa na inayoendelea, wasimamie kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kama ilivyopangwa kufikia mwaka 2025.




Post a Comment

0 Comments