Header Ads Widget

WANAFUNZI 70 WASHINDWA KUHUDHURIA MASOMO SHULENI KWA SIKU KUTOKANA NA UTORO




Afisa elimu Kata ya Didia Justus Bilago akizungumzia hali ya ukatili wa kijinsia katika eneo lake la kazi.

Stella Herman, Shinyanga Press Club Blog

  Mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi juu ya umuhimu wa kuchangia chakula mashuleni ili kuwawezesha watoto wao kupata chakula cha mchana kutokana na kuishi mbali na shule ,imekuwa ni chanzo cha wanafunzi kuwa watoro ambapo wastani wa wanafunzi 70 wanakosa masomo kwa siku.

Hayo yamebainika baada ya timu ya waandishi wa habari kutembelea shule ya sekondari Didia iliyopo Kijiji cha Bukumbi,wakati wakiwa katika utafiti wa masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na kuzungumza na wanafunzi pamoja na walimu.

Utafiti huo wa masuala ya ukatili wa kijinsia unafanywa na Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na mfuko wa wanawake Tanzania (WFT) ili kuhakikisha matukio yote ya ukatili wa kijinsia yanaibuliwa na kufanyiwa kazi ili kukomesha vitendo hivyo.

Mkuu wa shule ya sekondari Didia Mwalimu Faustine Magesa amesema wanafunzi wamekuwa wakishinda na njaa kuanzia asubuhi hadi saa 9.30 jioni muda wa kutoka shule,huku baadhi yao wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita kumi hadi kufika shule.

Amesema wanafunzi wanaposhinda na njaa wanakumbana na changamoto ya kujiingiza kwenye vitendo ambayo vimekuwa vikiharibu ndoto zao hasa kwa wasichana kurubuniwa na kuishia kupewa ujauzito na watu wanaowasaidia fedha.

“Ni kweli changamoto ni nyingi njiani ambazo wanakumbana nazo ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wengine kupata ujauzito na kwa mwaka jana 2020 wasichana wanne walipata mimba,pia wanatoka nyumbani alfajiri ili kuwahi shule wanaweza kunyanganywa hata baiskeli”alisema Magesa.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo akiwemo Haji Ramadhan na Irine Mponda wamesema changamoto ni kubwa kutokana na shule hiyo kujengwa mbali na makazi ya watu,ambapo njiani wamekuwa wakifiziwa na watu ili wachukuwe baikeli wanazotumia baadhi ya wanafunzi.

Mwanafunzi Irine amesema vishawishi ni vingi kwa watoto wa kike ambapo wavulana wanawasubiri njiani na kuwalazimisha kuwa na uhusiano wa kimapenzi jambo ambalo wamekuwa wakiripoti kwa walimu walimu wao na kisha kufanya ufuatiliaji ili kuwabaini.

Afisa elimu Kata ya Didia Justus Bilago alisema kulikuwa na ndoa za utotoni nyingi lakini baada ya elimu kutolewa hali imebadilika,ambapo wanafunzi na jamii nzima imekuwa na ushirikiano mkubwa wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili.

 Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Shinyanga Hoja Mahiba alisema anaitambua changamoto ya wanafunzi kusoma umbali mrefu na kwamba suala hilo wanalifanyia kazi na mkakati uliopo ni kujenga mabweni pamoja na shule nyingine ya sekondari.

Alisema matukio ya ukatili wa kijinsia bado yanaendelea kutokea maneo mbalimbali katika halmashauri hiyo zikiwemo ndoa na mimba za utotoni ambapo baada ya rikizo ya Corona mwaka 2020 wanafunzi 26 waligundulika kuwa na mimba. 


Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Didia halmashauri ya Shinyanga. 
Mkuu wa shule ya sekondari Didia Justine Magessa

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Didia halmashauri ya Shinyanga.

Mwalimu Charles Kaimkilwa anayesimamia malezi shuleni na Klabu ya wanafunzi wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
 

Post a Comment

0 Comments