Header Ads Widget

PROF. MANYA ATOA MAELEKEZO UTOAJI LESENI KWA MGODI WA MWIME 2 KAHAMA, ATAKA VIONGOZI KUMALIZA MGOGORO ULIOPO

Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya (katikati) akitoa maelekezo kwa viongozi wa mgodi wa Mwime uliopo mkoani Dodoma

Na Steven Nyamiti, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema migogoro yote inayohusu leseni za uchimbaji madini lazima zitatuliwe kupitia Tume ya Madini ambayo ndio taasisi yenye dhamana ya utoaji leseni hapa nchini wakati alipokutana na Viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Mwime 2 katika Ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Jijini Dodoma.

Prof. Manya amewataka viongozi wa Mgodi wa Mwime 2 kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini wakati wanapohitaji leseni kwenye maeneo ya uchimbaji ili kuondoa migogoro inayojitokeza mara mara.

Ametoa maelekezo hayo leo, Januari 25, mwaka huu alipokutana na viongozi wa Mgodi wa Mwime 2 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa mgodi huo kutoka Kahama mkoani Shinyanga ambao wamefika ofisini kwake kupata maelekezo ya sababu ya ucheleweshwaji wa maombi ya leseni ya Mgodi wa Mwime 2.

Naibu Waziri ametoa maelekezo hayo baada ya kuelezwa migogoro waliyonayo na Ofisi ya Madini wilaya ya Kahama kuhusu ucheleweshwaji wa kupatiwa namba ya malipo 'Control Number' kwa ajili ya kupatiwa leseni halali ya eneo la machimbo yaliyopo Mwime 2.

“Historia ya mgogoro wa Mwime 2 ni wa muda mrefu toka nikiwa kwenye nafasi ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini. Mimi ndiye niliyepitia leseni zenu tatu mnzazozitumia sasa. Kwa hiyo historia yenu yote ninaitambua. Ni vema mkafuata sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara kupitia watoa leseni Tume ya Madini,” ameeleza.

Aidha, Naibu Waziri amewataka viongozi hao wa mgodi wa Mwime 2 kusubiri kikao cha kamati ya wilaya ya Ulinzi na Usalama kitakachoongozwa na Mkuu wa wilaya mapema Februari, mwaka huu kwa ajili ya kutoa maamuzi ya mgogoro huo. Pia amewaeleza ili kuondoa migogoro hii mara kwa mara ni vyema kupokea maelekezo kutoka kwa afisa madini mkazi na kuyafanyia kazi kabla ya kuamua kuonana na Waziri mwenye dhamana kwanza.

Mhandisi Yahaya Samamba akipokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri amesema suala hilo analifahamu. “Ni vyema tukasubiri maelekezo ya kamati ya Ulinzi ya wilaya na kwa sababu nyinyi ndio watu wa mwanzo wa eneo hilo kuanza kufanya kazi nina imani mtapewa kipaumbele kuliko kugawa eneo kwa watu wageni kutoka nje ya Shinyanga”. Amesisitiza Sambamba

Naye, Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi wa Mgodi wa Mwime 2, Emmanuel Mlimandago amesema wanaiomba Tume ya Madini iwasaidie kutatua mgogoro huo ili wapate leseni ya kuendelea kuchimba katika eneo hilo.

“Tumeboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yanayozunguka mgodi wa Mwime 2, awali kulikuwa na changamoto ya mgodi kuingiliwa na maji lakini tuliweka juhudi ya ujenzi wa tuta kubwa ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kazi zetu,” Amesema Mlimandago

Pia, Afisa Mahusiano wa mgodi wa Mwime 2, Christopher Bundala amemuomba Prof. Manya kumuelekeza Kaimu Mtendaji wa Tume ya Madini, Yahaya Samamba kutembelea mgodi wa Mwime 2 wilayani Kahama ili mgogoro huo uweze kutatuliwa vizuri kwa kusikiliza pande zote za mgogoro huo kabla ya kutoa maamuzi.
Prof. Manya akisikiliza hoja za baadhi ya viongozi wa mgodi wa Mwime 2 waliofika ofisini kwake kueleza changamoto zinazowakabili
Kikao baina ya pande hizo mbili kikiendelea
Baadhi ya viongozi wa mgodi wa Mwime 2 wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya wakati wa kikao hicho

Post a Comment

0 Comments