Header Ads Widget

BITEKO AUTAKA UONGOZI MPYA TANZAM 2000 KUTIMIZA MASHARTI IKIWEMO KUWALIPA WANANCHI WA KATORO FIDIA

Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) pamoja na Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mubalwa (kushoto) na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahaya Samamba (kulia) wakiwa katika kikao na wadau wa madini na Kampuni ya Tanzam 2000

Na Greyson Mwase
WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko leo Januari 20, 2021 amekutana na uongozi mpya wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Dhahabu ya TANZAM 2000 jijini Dodoma uliofika kwa lengo la kujitambulisha.

Kikao hicho pia kimeshirikisha Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Madini, Edwin Igenge, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Madini,Tume ya Madini na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)

Wawakilishi kutoka katika kampuni ya TANZAM 2000 walikuwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu, Stephen Mullowney, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mradi, Giancardo Volo na Andrew Cheatle.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Biteko ameitaka kampuni hiyo kutimiza masharti yaliyowekwa ili kuondolewa kwa hati ya makosa waliyokuwa wameandikiwa na Tume ya Madini.

Masharti hayo yalikuwa ni pamoja na kupitia na kufanya marekebisho ya mpango kazi wa uendelezaji wa mgodi huo pamoja na kuwasilisha upya, kulipa fidia wananchi wanaozunguka mgodi huo katika eneo la Katoro mkoani Geita na kupitia na kufanya marekebisho ya mkataba kati yake na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)

Awali kampuni ya TANZAM 2000 ilisaini makubaliano mwaka 2011 na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Katoro Mkoani Geita, TANZAM 2000 ikiwa na hisa asilimia 45 na STAMICO hisa asilimia 55 lakini ikashindwa kuendeleza hali iliyopelekea kuandikiwa hati ya makosa na Tume ya Madini mwaka 2019.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini, Edwin Igenge (kulia) na Wataalam kutoka Tume ya Madini wakiwa sehemu ya kikao hicho

Wawakilishi wa Kampuni ya TANZAM 2000 wakifuatilia kwa umakini kikao hicho

Wawakilishi wa Wizara, Tume ya Madini na Kampuni ya TANZAM 2000 wakiendelea na kikao kilichoongozwa na Waziri Biteko


Post a Comment

0 Comments