Header Ads Widget

WAKAZI MTAA WA DOME MANISPAA YA SHINYANGA HATARINI KUKUMBWA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Nalinga Solomon (kushoto) na Mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Said Yusuph wakionyesha hali ilivyo katika ghuba (kituo) cha kuhifadhia taka kilichopo eneo la soko la Dome.

Na Suzy Luhende, Shinyanga
WAKAZI na Wafanyabiashara wanaozunguka Soko la Mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, wako hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu baada ya ghuba la kuhifadhia taka kujaa na kutirirsha maji machafu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, hivyo kusababisha harufu kali inayotokana na taka hizo ambazo hazijazolewa takriban mwaka mmoja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Shinyanga Press Club Blog baada ya kufika katika soko hilo kujionea hali halisi, baadhi ya Wafanyabiashara wa soko hilo akiwemo Magreth Emmanuel na Veronika Msengi wamesema wako hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kwa sababu ghuba (kituo) la kuhifadhi taka limejaa na kutiririsha maji machafu yaliyosambaa kwenye vibanda vyao na kuleta usumbufu.

Veronika ameeleza kuwa ni takribani mwaka mmoja sasa taka hizo zimekaa bila kuzolewa, na kwamba hali hiyo imefanya hata wakose wateja wa bidhaa zao kutokana na kero inayosababishwa na ghuba hilo.

"Walikuja kuzizoa mara moja tu wakaenda jumla, kwahiyo uchafu umerundikana kuanzia ule wa zamani na mpya na kusababisha hali iwe mbaya hadi sasa hayo maji yamebadirika rangi na kuwa ya njano na yamesambaa sehemu zote na tunakanyaga kila siku miguu inawasha sijui ndio fangasi tunapata shida sana," amesema Veronika.

Kwa upande wake, Stella Emmanuel ambaye ni mkazi wa mtaa wa Dome amesema kuwa awali alikuwa akifanya biashara ya kupika chakula na kuuzia wateja (mama lishe) lakini biashara hiyo ameiacha kwa sababu ya wateja kumlalamikia kwamba chakula chake kina harufu, hivyo kikawa hakinunuliwi na kwamba wamechoka na harufu hiyo kwani inaweza kuwaletea madhara makubwa kwa siku za baadae. 

"Sisi hatujasoma na sasa tunasomesha watoto wetu kupitia biashara hizi na sasa zimesima, tunaiomba Serikali itusaidie kuonda uchafu huu na haya maji, watusikie nasisi kilio chetu jamani, yakitokea magonjwa ya mlipuko hapa hatutaruhusiwa kuuza sasa tutaishije,"amesema.

Wakizungumzia hali hiyo, Wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Dome, Geleo Angelo na Said Yusuph wamesema kwamba wafanyabiashara wa soko hilo na wakazi wanapata shida kwani wamekuwa wakifika ofisini kutoa taarifa mara kwa mara, huku uongozi ukichukua hatua za kuitaarifu Manispaa lakini hakuna hatua za makusudi zinazofanywa kuuondoa uchafu huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Nalinga Solomon amesema ameshatoa taarifa mara nyingi manispaa lakini bado hakuna ufumbuzi uliofanyika, ambapo ameendelea kusisitiza kwa mamlaka husika kuingilia kati na kuona umuhimu wa kuwaokoa wananchi wake na hatari ya magonjwa ya mlipuko.

"Pia mitaro ya barabara inatakiwa kutengenezwa ili maji yasituame na yasisambae kuelekea kwenye majumba ya watu na walete vifusi vya molamu ili maji yasiendelee kutuama katika ghuba ni hatari kwa binadamu.

"Wafanyabiashara na wananchi wanaokaa karibu na soko hili wanapata shida hata kuhema tu kwa sababu hewa inayotoka kwenye ghuba hili ni nzito, malalamiko yanakuja ofisini kila siku na mimi nawafikishia wataalam lakini kimya, pia kuna maeneo mengine katika mtaa wetu ikiwemo East Mbezi kuna maji yanatoka msikitini hayana sehemu ya kwenda tunaomba mitaro ya kupitisha maji hayo," amesisitiza.

Akitolea ufafanuzi wa jambo hilo, Afisa Afya Manispaa ya Shinyanga, Kuchibanda Sinatus alipozungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu amesema suala hilo tayari ana taarifa nalo na litaanza kufanyiwa kazi kuanzia kesho (Jumanne).
Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Nalinga Solomon akionyesha namna ambavyo ghuba hilo limeleta kero kwa wananchi wake 
Baadhi ya wananchi wakijionea hali halisi ilivyo katika ghuba hilo lililopo karibu na soko la mtaa wa Dome

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dome, Nalinga Solomon akionyesha maji machafu yaliyokaa muda mrefu ambayo yanaleta harufu kali na kero kwa wananchi wake

Mfanyabiashara wa Mboga na Matunda katika soko la Mtaa wa Dome, Stella Emmanuel akizungumza na mwandishi wa habari hii namna ambavyo taka hizo zimekuwa kero na kufanya wateja wakosekane. 

Post a Comment

0 Comments