Header Ads Widget

WATANO WASHIKILIWA SHINYANGA TUHUMA ZA KUHARIBU MALI VURUGU ZA CHADEMA NA CCM, MAANDAMANO BAADA YA KAMPENI YAKATAZWA



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Shinyanga Press Club Blog 
JESHI Polisi mkoani Shinyanga linawashilikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kujeruhia na kuharibu mali wakati wa mvutano na vurugu za wafuasi wa vyama vya Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Shinyanga Mjini. 

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 25, 2020 mjini Shinyanga na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambapo amebainisha kuwa vurugu hizo zilitokea Jumamosi Oktoba 24, mwaka huu wakati wagombea wa nafasi za ubunge wa jimbo hilo, Patrobass Katambi wa CCM na Salome Makamba wa Chadema walipokutana wakati wakitoka kwenye mikutano yao ya kampeni. 

Akielezea tukio hilo, Kamanda Magiligimba amewataja waliokamatwa kuwa ni Ramadhan Mohammed (20) mkazi wa Ndembezi, Y uda Kanoku (22) mkazi wa Ibadakuli, Frank Chiza (20) mkazi wa Kahama, Timoth Amos (20) mkazi wa Ibadakuli na Mussa Luhende (21) mkazi wa Ibadakuli wakituhumiwa kwa makosa ya kujeruhi na kuharibu mali. 

Ambapo vurugu hizo zilisababisha majeraha kwa baadhi ya watu akiwemo Hasani Masanja (28) mkazi wa majengo aliyejeruhiwa na kitu chenye ncha kali kidevuni akiwa na gari alilokuwa anaendesha lenye namba za usajili T 786 BEK Toyota Noah gari ya matangazo ya mgombea ubunge CCM nalo lilivunjwa vioo vyote, pia Doto Joshua (29) mkazi wa Lubaga alivunjiwa kioo cha gari cha mbele ikiwa na namba za usajili T 444 CFA Suzuki Swift, pia Secilia Sangaluka (42) alivunjiwa taa indicator ya nyuma kushoto. 

“Jana Jumamosi majira ya saa moja jioni wakati wagombea wa nafasi ya ubunge jimbo la shinyanga mjini wa CCM na Chadema wakiwa wanarudi kutoka kwenye maeneo ya kampeni zao wakielekea katika ofisi zao za vyama vya siasa walikutana katika eneo la Japanise Corner na vurugu zikaanza katika eneo hilo…. watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,” amesema. 

ACP Magiligimba ametoa wito kwa wanasiasa pamoja na wafuasi wao kuacha kufanya siasa za vurugu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na wafanye kampeni zao kwa amani na utulivu na mara baada ya mikutano kumalizika wananchi wanatakiwa kutawanyika na si kufanya maandamano kuelekea kokote kule.

Post a Comment

0 Comments