Header Ads Widget

NJEMBA YANASWA NA KICHWA CHA MTOTO MBELE YA BUNGE


Polisi nchini Uganda wametibitisha kuwa kichwa cha mtoto kilichokatwa, kilichopatikana katika kikapu cha mwanaume aliyekamatwa kwenye lango la bunge nchini Uganda Jumatatu, kilikuwa ni sehemu ya mwili uliopatikana katika wilaya ya Masaka, kusini- magharibi mwa mji mkuu Kampala.

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai nchini humo inasema wachunguzi watafanya kipimo cha vinasaba DNA kwa wajumbe wa familia moja ya Masaka ambao waliripoti kupotea kwa mtoto wao, kubaini iwapo kweli mtoto huyo aliyekatwa kichwa ni wao.

Familia iliyompoteza mtoto iliviambia vyombo vya habari nchini humo Jumanne, kwamba walikuwa wamemuajiri Joseph Nuwashaba, mwenye umri wa miaka 22, ambaye alipatikana na kichwa cha mtoto, kama mfanyakazi wa shamba lao.

Uchunguzi bado unaendelea kubaini ni yapi yalikuwa malengo ya Bwana Nuwashaba, na polisi wamesema watafanya uchunguzi juu wa akili yake.

Alipokamatwa Bwana Nuwashaba aliwaambia maafisa katika bunge kwamba alitaka kuwasilisha mzigo uliokuwa na kichwa kwa Spika wa Bunge Bi Rebecca Kadaga.

Spika hajatoa kauli yoyote juu yatukio hilo, na aliwaambia wabunge kuwa anasubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi.