TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp +255 789 632 732, +255 756 546 015 au +255 686 057 440

NCHAMBI AMNADI MGOMBEA UBUNGE KISHAPU AWATAKA WANANCHI KUMPA KURA ZA KISHINDO


Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu Boniface Butondo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nobora Kata ya Talaga wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi wa kampeni.


Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni Kijiji cha Nobora wilaya ya Kishapu.


Suzy Luhende, Shinyanga
ALIYEKUWA. mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi amemuombea kura mgombea ubunge wa Jimbo hilo kupitia chama Cha mapinduzi CCM Boniface Butondo na kuahidi kushirikiana nae ili aweze kupata ushindi wa kishindo.
Ombi hilo amelitoa leo kwenye uzinduzi wa kampeni ya mbunge Boniface Butondo, uliofanyika kijiji cha Nhobora kata ya Talaga wilayani Kishapu, ambapo alisema anawaomba wananchi wote wa Jimbo la Kishapu kumpa kura zote Butondo ili aweze kushinda kwa kishindo.


Alisema amewatumikia wananchi kwa muda wa miaka 10 hivyo hana budi kukabidhi kijiti kwa Butondo ili aendeleze gurudumu la maendeleo katika wilaya ya Kishapu.


"Ndugu zangu wanakishapu nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu mlionipatia wakati nikiwa mbunge kwa miaka 10, Sasa naomba mmpe ushirikiano Butondo kwani sitaki kuona Kura hata moja inaenda upinzani, zote tumpigie diwani wa kata hii mbunge wa chama Cha mapinduzi pamoja na Rais John Pombe Magufuli"amesema Nchambi.

Amesema Jimbo la Kishapu halitabadilika kwa sababu aliyemwachia Ni mchapa kazi lakini litaongezeka kimaendeleo, kwa sababu anamjua vizuri, kwani wameshirikiana nae wakati akiwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kufanya maendeleo ikiwemo kujenga barabara, na kutatua changamoto mbalimbali, hivyo anaamini ataendelea kufanya makubwa zaidi.

"Nimekuwa kimya kwa kipindi kirefu si kwamba nimezila naahidi kwamba nitashirikiana nae Butondo na kuhakikisha chama Cha mapinduzi kinachukua dola, na nitakuwa nae bega kwa bega na kushirikiana na CCM siku zote za maisha yangu,kwa sababu mmenitoa katika migongo yenu na mmenishauri mengi"amesema Nchambi.

Alisema atashirikiana na Viongozi wote wa chama Cha mapinduzi ili kuhakikisha Jimbo la Kishapu linapata kura nyingi za kutosha na kuhakikisha Kishapu inaongoza kwa Kura nyingi kuanzia kwa madiwani mbunge na kwa Rais.

Kwa upande wake mgombea ubunge Boniface Butondo aliwaomba wananchi wote wa Kishapu wamchague ili aweze kuwatumikia kwani anajijua yeye ni mchapakazi mzuri katika kudimamia maendeleo.

Amewaomba wananchi wa Jimbo hilo wakiamini chama Cha mapinduzi kwani kimefanya Mambo makubwa yakiwemo ya sekta ya elimu,ambapo serikali kupitia chama Cha mapinduzi imejenga madarasa, imetengeneza madawati na kujenga nyumba za walimu.


Butondo amesema pia serikali kupitia chama Cha mapinduzi imejenga zahanati katika kata mbalimbali na vijiji na itaendelea kupanua vituo vya afya ili kina mama wenye matatizo mbalimbali yakiwemo ya upasuaji wahudumiwe ndani ya wilaya.


Aidha amesema akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha kina mama wanakopeshwa ile asilimia nne, vijana asilimia nne na walemavu asilimia mbili ili waweze kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.

"Tayari serikali kupitia chama cha mapinduzi Jimbo la Kishapu imeshatoa mikopo kwa vikundi saba ambavyo vinajishughulisha na ufugaji wa kuku na baadhi ya vijana wameshakopeshwa piki piki kwa ajili ya kufanya boda boda ili kujipatia ridhiki"amesema.

Alisema katika sekta ya maji, atahakikisha maji ya ziwa Victoria yanasambazwa katika kata zote za Kishapu, ikiwa Ni pamoja na huduma ya umeme kusambazwa vijiji vyote vya Jimbo hilo.
"Wapendwa wananchi wangu naomba Sana mmpe Kura zote Rais Magufuli na mmpe Kura zote diwani wa kata hii na upande wa ubunge nipeni Mimi ili niweze kuwaletea maendeleo kwa kushirikiana na Rais wangu mpendwa, mchapa kazi John Pombe Magufuli,"aliongeza Butondo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama Cha mapinduzi CCM Mabala Mlolwa aliwaomba wananchi wanaochonganisha waache mara moja wamuache mbunge aliyemaliza mda wake ashirikiane na mbunge mteule wafanye kazi za chama kama timu.


Mbunge wa Viti maalum Lucy Mayenga akimuombea kura mgombea Ubunge jimbo la Kishapu Boniface Butondo.
Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu akiendelea kuomba kura kwa wananchi
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi akimuombea kura mgombea Ubunge wa Jimbo la Kishapu Boniface Butondo
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni


Mkutano wa uzinduzi wa kampeni unaendelea