TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp +255 789 632 732, +255 756 546 015 au +255 686 057 440

WANANCHI KAHAMA WAKUMBWA NA TAHARUKI BAADA YA LORI LA MAFUTA KULIPUKA NA KUJERUHI


Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa Kahama Mjini.
Na Salvatory Ntandu .Shinyanga Press Club Blog 
Kijana ambaye jina lake halijafahamika mara moja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-30 amenusurika kifo kwa kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya mfuniko wa tenki la mafuta la gari lenye namba za usajili namba T 393 BEZ kulipuka katika eneo la Bijampola Mjini Kahama likifanyiwa matengenezo.
Wakizungumza na Malunde 1 Blog baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Baraka John amesema kuwa akiwa katika eneo lake la kazi majira ya saa tatu asubuhi leo Jumapili Agosti 9,2020 wakati mafundi wa kuchomelea magari wakiwa wanalifanyia matengenezo gari hilo ghafla lililipuka na kusababisha madhara mbalimbali.

Amesema Mafundi waliokuwa wanatengeneza gari hilo hawakuchukua tahadhari ili kujiridhisha kama kuna mafuta yaliyosalia kabla ya kuanza kulichomelea hali iliyosababisha kujitokeza kwa mlipuko huo ambao umesababisha majeruhi mmoja na kuharibu mali mbalimbali katika eneo hilo ikiwemo vibanda na nyumba.

“Magari kama haya yanayobeba vimiminika vinavyolipuka ni bora yakazuiwa kufanyiwa matengenezo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu au kwenye makazi ya watu,serikali ipige marufuku uchomeleaji wa magari haya mitaani kwani ni hatari kwa usalama,”amesema John.

Naye Joyce Paulo anayejihusisha na shughuli ya kuuza vyakula 'Mamalishe' katika eneo la Bijampola amesema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwani mlipuko huo ulikuwa ni mkubwa na baadhi ya vyuma vilikuwa vinaruka katika maeneo mbalimbali huku moshi mkubwa ukiwa unasambaa kwa kasi katika makazi ya watu.

“Tulidhani ni bomu limelipuka katika eneo letu kwani nyumba ya jirani yetu imeharibiwa sana na baadhi ya vyuma vilivyokuwa vinajitokeza baada ya kulipuka,tunaiomba serikali idhibiti uegeshaji ovyo wa magari yenye mafuta katika eneo hili,”amesema Joyce.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Dk Lucas David amethibitisha kupokea majeruhi mmoja ambaye ametokana na ajali ya kulipuka kwa tanki la Mafuta iliyotokea leo katika eneo la Bijampola ambaye amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na anaendelea kupatiwa matibabu.

“Kwa sasa amepelekewa katika chumba cha X-ray kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi,anaonekana amepata mivunjiko katika maeneo mbalimbali ya mwili wake",amesema Dk. David.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio na kwamba atatoa taarifa rasmi.
Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa

Nyumba ikiwa imeharibika baada ya mfuko wa tanki la mafuta kuripuka gari likitengenezwa