TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp +255 789 632 732, +255 756 546 015 au +255 686 057 440

EMIRATES YAKANYAGA ARDHI YA TANZANIA.


NDEGE Ya Shirika Emirates EK 725 tayari imeshatua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere mapema jumamosi majira ya saa saba na dakika ishirini huku ikielezwa kuwa baada ya janga la Covid-19 sasa shirika hilo limerejea ili kutoa huduma zao za kimataifa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi mkazi wa Shirika hilo nchini Majid Al Falasi imeelezwa kuwa safari za Tanzania na Dubai zitakua mara mbili kwa wiki kupitia Emirate's Boeing 777-300ER na wateja wanaweza kupata tiketi zao kwa wakala wa usafiri au kwa njia ya mtandao.

"Tunafurahi kujeresha na kuendelea kutoa huduma nchini Tanzania na tumeendelea kujenga mahusiano bora na nchi pamoja na wateja wetu kwa miaka 20 sasa, tunapenda kuchukua nafasi hii kuzishukuru Mamlaka kwa ushirikiano mzuri wanaoonesha katika utoaji wa huduma hii" ameeleza Falasi.

Aidha amesema kuwa baada ya kufungua safari za Dubai kwa wasafiri wa Tanzania bado wamekuwa wakizingatia na kuchukua hatua zaidi za kiafya kwa wateja na waajiriwa wa shirika hiyo katika kujiweka salama zaidi na virusi vya Corona (Covid-19.)

Amesema kuwa kwa mwezi huu Emirates imepanua mtandao wake  kwa maeneo 68 zaidi huku maeneo 7 yakiwa barani Afrika ikiwa ni pamoja na kutoa mwanya kwa wateja wao duniani  kutembelea maeneo mengi zaidi kupitia Dubai.

Shirika la ndege la kimataifa la Emirates lilianzishwa mwaka 1984 na mwaka 1987 lilimiliki ndege yake ya kwanza ya Airbus A310 na baadaye kutambulika kimataifa katika utoaji wa huduma bora za anga, na wiki iliyopita Emirates lilikuwa Shirika la kwanza kutoa huduma za Covid-19 kwa wateja wao ikiwemo gharama za matibabu pamoja na karantini.