Header Ads Widget

SH MIL. 13.01 ZAKUSANYWA UJENZI WA MADARASA, NYUMBA ZA WATUMISHI BUBALE –SHINYANGA


Mojawapo ya madarasa yanayojengwa katika mpango wa kupunguza tatizo la vyumba vya madarasa shule ya msingi Bubale.

Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog

JUMLA ya Sh Milioni 13,014,400 zimekusanywa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba 9 vya madarasa, ofisi mbili za walimu na nyumba ya mganga (two in one) katika kijiji cha Bubale pamoja na darasa la awali katika kitongoji cha Mwamnyepe, iliyoshirikisha wananchi, watendaji, wadau mbalimbali na viongozi wa serikali wilaya ya Shinyanga.

Harambee hiyo imefanyika leo Julai 11, 2020 shule ya Msingi Bubale Kata ya Masengwa Tarafa ya Samuye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, imengozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Jasinta Mboneko, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba na watendaji wengine kutoka halmashauri hiyo.


Ambapo, DC Mboneko amechangia Sh Milioni1, halmashaur i ikachangia Sh Milioni 5 na Mkurugenzi akachangia mifuko 20 ya Saruji, Mganga Mkuu wa wilaya na timu yake walichangia  Sh 790,000, Serikali ya Kijiji Sh 86,500, Jeshi la Sungusungu likiahidi Sh 50,000 na mifuko 20 ya saruji na ofisi ya Afisa Elimu Msingi ikiahidi Sh 200,000.


Hivyo fedha taslimu zilizokusanywa ni Sh 1,379,900, ahadi zikiwa Sh 7,050,000, saruji mifuko 189 yenye thamani ya Sh 3,496,500, Mbuzi mmoja mwenye thamani ya Sh 50,000 na ahadi ya kuwekewa madirisha ya vioo (Alumnium) kwenye nyumba ya mganga inayojengwa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
  
Akizungumza wakati wa kuzindua harambee hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ameupongeza uongozi wa kata hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuleta maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali, ambapo serikali itaendelea kuwa nao bega kwa bega kwa kuwaletea mganga katika zahanati ya kijiji hicho, kutatua kero ya umeme na maji na kuhakikisha majengo hayo yanajengwa kwenye ubora unaotakiwa.


DC Mboneko amewataka pia wananchi hao kuhakikisha watoto wanahudhuria shuleni na wale wote walio na mpango wa kuozesha wanafunzi basi waache mara moja, huku akiwasihi kutouza chakula chote na kumaliza akiba nyumbani.


“Nilifika hapa mwaka jana kwenye mkutano wa wananchi, hii ni hatua nzuri mliyoipiga leo tunakutanishwa tena hapa kwa shughuli ya maendeleo, kwahiyo nawapongeza wananchi kwa kujitoa kwenu kuchangia ujenzi huu na Mhandisi wetu atakuja kusimamia hapa ili majengo yetu yawe bora.


“DMO yuko hapa naye atahakikisha analeta mganga nyumba ikikamilika, tunapoendelea kujenga majengo haya basi tuyakamilishe na serikali itaweka nguvu zake, kwahiyo kwa wale ambao wana mpango wa kuozesha watoto basi mpango huo ufe na wanafunzi hao waende shule,” amesema DC Mboneko.

 Mkurugenzi Mtednaji wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba amewapongeza wananchi hao na kuwaeleza kuwa serikali inatambua jitihada wanaznazozifanya  na itakuwa nao kuhakikisha adhma hiyo chanya inatimizwa, ambapo aliwaomba watendaji wengine wa vijiji vitatu vya Ikonda, Ilobashi na Masengwa katika kata hiyo kuiga mfano wa Bubale.


“Ahsanteni wana Bubale kwa juhudi kubwa mnazozifanya ni dhahiri kwamba mnaunga mkono jitihada za serikali katika kulenda maendeleo na mnakerwa na changamoto zilizopo na sisi tunatambua jitihada zenu, hivyo serikali itakuwa pamoja nanyi,” amesema.

 Afisa Mtendaji Kata ya Masengwa, Hussein Majaliwa

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili kata yake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Masengwa, Hussein Majaliwa amesema shule ya Bubale yenye wanafunzi 1,175 wavulana 657 na wasichana 528 inao uhitaji wa madarasa 24, yaliyopo ni 9 na upungufu ni 15, nyumba za walimu mahitaji ni 24, zilizopo ni 4 pekee na upungufu ni nyumba 20.


Kwa upande wa matundu ya vyoo, mahitaji ni 52, yaliyopo ni 12 na upungufu ni 40, huku mahitaji ya walimu yakiwa 24 na waliopo wakiwa 12 tu, ambapo zahanati hiyo inao manesi wawili peke yake ikiwa haina mganga, hivyo ameiomba serikali kusaidia kuleta mganga pale nyumba hiyo ikikamilika.


Majaliwa amesema ujenzi wa vyumba vya madarasa 9, darasa la awali, ofisi na nyumba ya daktari umeanza kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho, ambapo shule imechangia Sh 500,000, zahanati 25,000 na mifuko mitatu ya saruji, serikali ya kijiji ikichangia Sh 70,000 na mifuko 40 ya saruji, huku jeshi la Sungusungu likichangia Sh 1,940,000 na mifuko 200 ya saruji na kufanya jumla ya michango mbalimbali ni Sh 2,535,000 na mifuko 264 ya saruji.


“Jamii imeshiriki kwa kupakia mchanga tripu 25, kuchimba msingi, kusomba maji, kumwagilia, kumwaga zege na kusimamia mafundi, tunawashukuru kwa kufika hapa na kuja kutuunga mkono,” amesema.
 Viongozi mbalimbali wa serikali waliohudhuria harambee hiyo wakifurahia jambo
 Mwenyekiti wa Sungusungu katika kijiji hicho, Moses Jidai
 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hoja Mahiba na Afisa Tarafa ya Samuye,Ntarle Magese wakiwa kwenye msafara kukagua eneo inapojengwa nyumba ya daktari katika kijiji cha Bubale.

 Msingi utakaotumika kujenga nyumba ya daktari katika zahanati ya kijiji cha Bubale Kata ya Masengwa.
 Afisa Mtendaji Kata ya Masengwa, Hussein Majaliwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya, Jasinta Mboneko
 
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Bubale, Phantom Nkonoki
Wananchi wa kijiji cha Bubale wakifuatilia harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule ya kijiji hicho.

 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akifurahia jambo na Afisa Tarafa ya Samuye, Ntarle Magese
 DC Mboneko akipokelewa baada ya kuwasili katika kijiji cha Bubale
 Afisa Tarafa ya Samuye, Ntarle Magese (kulia) akitoa maelezo mbalimbali kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko

Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Dk. Mameritha Basike akizungumza katika harambee hiyo.
 Kaimu Afisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, Christina Bukori
 DC Jasinta Mboneko akicheza na jeshi la Sungusungu wakati wa hafla hiyo

 Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Hoja Mahiba na Mganga Mkuu wa halmashauri, Dk. Mameritha Basike wakicheza pamoja na jeshi la sungusungu la kijiji cha Bubale wakati wa hafla ya harambee kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
 
 Viongozi wakifuatilia risala iliyokuwa ikisomwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Masengwa, Hussein Majaliwa

 Afisa Mtendaji wa Kata ya Masengwa, Hussein Majaliwa akimkabidhi risala, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko

 DC Jasinta Mboneko akisisitiza jambo kwa wananchi