Header Ads Widget

MAKADA 181 CCM WACHUKUA FOMU ZA UBUNGE MAJIMBO MANNE MWANZA



BAADA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufungua pazia la uchukuaji wa fomu za kinyang’anyiro cha ubunge na udiwani kwenye majimbo na kata mbalimbali nchini jana, utitiri wa makada umejitokeza kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na chama hicho tawala kugombea ubunge kwenye majimbo ya Mkoa wa Mwanza.
Katika Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, idadi ya wana CCM 47 wanatajwa kujitokeza kuchukua fomu kati ya watia nia 75, ambapo watatu kati ya 47 waliochukua fomu wamerejesha fomu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga , amesema jana kwamba kwenye Jimbo la Nyamagana makada 47 wamechukua fomu na watatu tayari wamerejesha.
Waliorejesha fomu hizo ni mbunge anayemaliza muda wake, Stanslaus Mabula, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iringa, Robert Masunya na John Fransisco Nzilanyingi.
Katika majimbo ya Sumve na Kwimba wamejitokeza wana CCM 70 kuchukua fomu za kuwania ubunge kwenye majimbo hayo mawili ya Wilaya ya Kwimba na waliochukua fomu katika jimbo la Kwimba ni mbunge aliyemaliza muda wake, Shanif Mansoor, Dkt. Peter Mugasha, Mary Onesmo Kalumbete, Mary Stephano Sakila, Yusufu Sakila, Dkt. Lawrent Nyanda Kombe na Shilogela B. Nganga.
Kwenye Jimbo la Sumve baadhi ya waliokwishajitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge wa jimbo hilo ni Peter Ngusa, Dkt. Kusekwa Longino, John Bugarana, Ng’umbi, Moses C .Bujaga, William Peter Ndila, Zephania Paul Wanga Masangu na Profesa John Mahugija.
Kwa upande wa Jimbo la Ilemela Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela Aziza Isimbula amesema jumla ya makada 41 wamejitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ndani ya chama ya nafasi ya Ubunge akiwemo Mbunge anayemaliza muda wake, Dkt. Angeline Mabula ambaye amejitosa kuwania kiti hicho kwa mara ya pili baada ya kuchukua fomu jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson Mesha.


Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Magu, Waridi Mngumi amesema jumla ya makada 23 wamejitokeza jana kuchukua fomu akiwemo aliiyekuwa Mbunge wa jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga ambaye amechukua na kurejesha fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo hilo.
Kiswaga aliwasili muda wa saa 2:00 asubuhi jana Julaibe14 mwaka huu katika ofisi za CCM Wilaya ya Magu na kuchukua fomu za kuomba kuwania ubunge katika chama na baada ya kukamilisha kujaza hatimaye saa 6 mchana wa siku hiyo alifanikiwa kurejesha.