Header Ads Widget

KATAVI: MME AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUUA MKE NA WATOTO WAKE WAWILI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga imemhukumu, Yustine Robart (35) kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuuwa mkewe, Jackilina Lwiche na watoto wake wawili, Frenk Robart (4) na Elizaberth Robart (6).

Mtuhumiwa huyo baada ya kuua mke na watoto wake hao wa kuzaa aliwatumbukiza kwenye kisima cha maji.

Hukumu hiyo ilitolewa leo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, David Mrango katika kikao cha Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga kinachoendelea kusikiliza kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Katavi iliyoko Manispaa ya Mpanda.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya mahakama kuridhika pasipo shaka lolote na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashahidi wanne .

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali,  Lugano Mwasubira na mshtakiwa alikuwa akitetewa na wakili Patrick Mwakyusa.

Awali katika kesi hiyo, Wakilii wa Serikali Mwasubira ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa, Robart alitenda kosa hiloAgosti 5, mwaka 2013 saa nne usiku katika Kijiji cha Maji Moto Wilaya ya Mlele  Mkoa wa
Katavi.

Amedai kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo mshtakiwa alikuwa na ugomvi na marehemu mke wake ambaye alikuwa akiishi naye muda kwa miaka sita kama mume na mke.

Amedai baada ya ugomvi huo kutokea alimfukuza mkewe ili aondoke nyumbani kwake walipokuwa wakiishi na watoto wao watatu kwenye nyumba ya kupanga kijijini hapa.

Mwasubira amesema baada ya ugomvi uliibuka mgogoro wa kugawana vyombo vya ndani, ambapo mshtakiwa alimruhusu marehemu kuchukua vyombo vya ndani isipokuwa asichukue jagi .

Hata hivyo marehemu alikaidi maagizo hayo ndipo alipochukua jagi hilo na kulivunja kitendo ambacho kilimkasirisha mshtakiwa ambapo alimpiga huku akiahidi kwamba atahakikisha atamfanyia kitu kibaya ambacho kitakuwa ni historia kwenye kijiji hicho, kwani kitakuwa hakijawahi kutokea.

Mwasubira amesema baada ya hapo marehemu hakuonekana kwenye nyumba hiyo na watoto wake wawili. Amesema ilipofika kesho yake saa nne asubuhi ndipo walipompata mtoto mdogo wa miaka miwili akiwa hai.

Kwa mujibu wa wakili huyo mtoto huyo alikutwa akiwa ametelekezwa kwenye kichaka na wanakijiji waliweza kumtambua kuwa ni moto wa mshtakiwa.

Amesema majirani walianza kumtafuta marehemu pamoja na watoto wake wawili, Frenk Robart na Elizabert Robart na walifanikiwa kuwaona wakiwa ndani ya kisima cha maji kilichokuwa umbali wa mita mia mbili kutoka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi wakiwa wamefariki.

Mshtakiwa, Yustine katika utetezi wake ameiomba Mahakama imwachie huru kwa kile alichodai kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha ushahidi kuwa yeye alihusika na mauaji hayo.

Madai hayo yalipingwa na Wakili Mwasabira ambaye amedai kuwa ushahidi wa mazingira unaonesha kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda Sumbawanga, David  Mrango amesema katika kesi hiyo hakuna shahidi aliyethibitisha kwa ushahidi kuwa alionekana akifanya kitendo hicho, isipokuwa kesi hiyo imejengwa kwa ushahidi wa mazingira na Mahakama
mbalimbali kama vile Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Afrika Mashariki zimewahi kutoa maamuzi ya kesi kama hiyo kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira.

Amesema miongoni mwa ushahidi wa mazingira uliotolewa kwenye kesi hiyo
unaomfanya mshtakiwa atiwe hatiani ni kauli yake aliyoitoa  kuwa atamfanyia marehemu kitu kibaya cha historia kijijini hapo.

Ameongeza kuwa licha ya mke na watoto kutoonekana nyumbani, hakuonesha juhudi za kuwatafuta wala kutoa taarifa kitu ambacho sio cha kawaida kwa binadamu.

“Hivyo Mahakama imeona hakuna ubishi wowote unaonesha kuwa mshtakiwa
Yustine Robart hakufanya mauaji hayo ya mke wake na watoto wake
wawili, hivyo Mahakama imemtia hatiani kwa kosa la kifungu cha sheria
Namba 16 (1) cha kanuni ya adhabu,”
amesema.

SOMA ZAIDI>>>>